Home Head On Gender Watumitizi wa mihadarati miongoni mwa wanaoishi na ulemavu waongezeka.

Watumitizi wa mihadarati miongoni mwa wanaoishi na ulemavu waongezeka.

545
0

Changamoto kuu ikisalia kuwa miundo msingi hususan katika kukabiliana na donda sugu la mihadarati nchini, athari yake inaendelea kudidimiza wananchi wengi haswa vijana huku idadi ya walemavu wanaojitosa katika dibwi hilo ikiripotiwa kuongezeka.

Unyanyapaa, kukataliwa na jamii, ukosefu wa nafasi za ajira ni miongoni mwa sababu zilizotajwa kuchangia pakubwa kwa walemavu kuingilia matumizi ya mihadarati kwa nadharia ya kujiliwaza ila ndio mwanzo wa maangamizi yao.

Akizungumza na wanahabari wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya watu wanaoishi na ulemavu, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kurekebishia tabia la Reach Out Centre Trust, Taib Abdurahman amebaini kuwa kumekuwa na ongezeko la watumizi wa mihadarati miongoni mwa watu wanaoishi na ulemavu.

“tangu tuanzishe mradi mahasusi unaolenga kuwafikia watumizi wote wa mihadarati katika kaunti ya Mombasa, idadi ya wanaotumia mihadarati miongoni mwa walemavu imeonekana kuongezeka,” alisema Taib.

“Kufikia sasa, tumesajili takriban watu 20 wanaoishi na ulemavu ambao wanaendelea kupata matibabu na ushauri nasaha katika kituo chetu,” aliongezea Bw. Taib.

Vile vile alielezea changamoto iliopo ni kuwa baadhi ya wanaoishi na ulemavu kushindwa kuvifikia vituo mbali mbali vya kubadilishia tabia licha ya kampeini ya huduma za bure zinazoendelezwa kupitia mashirika tofauti pamoja na wizara ya afya kaunti ya Mombasa.

Hata hivyo kwa upande wake afisa katika baraza linaloshughulikia maswala ya wanaoishi na ulemavu nchini Juliet Ruwa amedokeza kukabiliana na changamoto za kuhakikisha huduma mbali mbali zinawafikia wanaoishi na ulemavu kwani wengi wao wanasusia kusajiliwa.

Afisa katika baraza linaloshughulikia maswala ya wanaoishi na ulemavu nchini Juliet Ruwa akizungumza na wanahabari jijini mombasa. Picha/Husseiny Mduney

3277 pekee wamesajiliwa kutoka kaunti ya Mombasa idadi ambayo inasadikika kuwa ya chini kulingana na baraza hilo.

Aidha amebaini kuwa usajili huo utasaidia pakubwa katika kuwatambua raia wa humu nchini dhidi ya wale wa kigeni hatua ambayo itarahisisha utoaji wa huduma za kiafya, elimu miongoni mwa nyinginezo.

Mkurugenzi wa maswala ya jinsia katika idara ya Vijana,Jinsia,Michezo na utamaduni katika kaunti ya Mombasa Esther Ingolo ametilia mkazo umuhimu wa kukabiliana na dhulma za kijinsia katika jamii.

Bi Esther amedokeza dhulma hizo zimeathiri wengi kiasi cha kupelekea wengine kujitoa uhai jambo ambalo amesisitiza kuwa iwapo halitakemewa haki zitaendelea kukiukwa na kusambaratisha jamii.


Aidha amebaini kuwa takwimu zimeashiria wanawake hudhulumiwa zaidi huku idadi ikiripotiwa kuongezeka miongoni mwa watu wanaoishi na ulemavu.

“lazima tujikakamue kuona kuwa visa vya dhulma za kijinsia vinasitishwa kwa njia moja ama nyengine hususan kwa watu wanaoishi na ulemavu ambao wamekuwa wakinyimwa haki zao,” alisisitiza Bi.Esther.

Dhulma kama hizi ndio chanzo kikuu kwa baadhi kujitosa katika matumizi ya dawa za kulevya.