Home News NTSA yashinikizwa kuhusisha wadau kuunda mfumo mpya

NTSA yashinikizwa kuhusisha wadau kuunda mfumo mpya

493
0

Kuna haja ya kuhusisha wadau katika sekta ya uchukuzi ikiwemo shule za udereva katika mchakato wa kuainisha mfumo mpya wa masomo ya udereva kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa shule za udereva ukanda wa pwani John Magara akishinikiza kuwa mamlaka ya kudhibiti uchukuzi na usalama wa barabarani NTSA haina budi ila kushirikiana vyema na taasisi mbali mbali za kutoa mafunzo ya udereva ili kuhakikisha kuwa mapendekezo katika rasimu yanapigwa msasa.

Akitoa dukuduku zake, mwenyekiti huyo amebaini kuwa kutumika kwa baadhi ya sheria hizo mpya za barabarani bila ya kutoa hamasa ya kutosha kwa wahusika na wadau wa sekta hiyo ya uchukuzi kumepokelewa kama ukiukaji wa haki hasa ikizingatiwa kuwa wengi hawana ufahamu kamili wa sheria hizo.

“tumekuwa tukipokea malalamishi mengi kutoka kwa maderava kuhusiana na kusumbuliwa na maafisa wa trafiki kuhusiana na sheria za rasimu hiyo,” alisema Magara.

Aidha mwenyekiti huyo alidokeza kutoupigia debe mfumo huo mpya iwapo wadau hawatajumuishwa katika mchakato mzima wa kuunda mfumo huo wa masomo ya udereva nchini.

“hatuwezi kukubali kulimbikiziwa sheria na mfumo ambao hatujahusishwa kikamilifu, lazima maoni ya wadau na wahusika yachukuliwe na kujadiliwa. Iwapo hatua hiyo haitafuatwa basi tutaandika barua kwa kamati ya bunge la kitaifa kupinga rasimu hiyo,” alikariri mwenyekiti huyo.

Hata hivyo kwa upande wake naibu mkurugenzi wa usalama wa barabarani katika mamlaka ya NTSA Duncan Kibogong Cheriyot amekanusha madai ya kutotambulika kwa rasimu hiyo miongoni mwa wadau huku akidokeza kuwa tayari zoezi la kukusanya maoni linaendelea.

“hatuwezi kuweka sheria mpya bila ya kuhusisha wadau wa sekta ya uchukuzi, ndiposa tumeanzisha zoezi la kukusanya maoni ili kutafuta njia mwafaka na kubuni mtaala bora wa masomo ya udereva utakaokubalika na wengi” alisema bw. Duncan.

Itakumbukwa kwamba mamlaka ya kudhibiti uchukuzi na usalama barabarani NTSA ambayo inatekeleza majukumu yake chini ya wizara ya usalama wa ndani inajizatiti kupunguza maafa na ajali huku ikistawisha usalama wa wananchi barabarani.