Home Swahili Hub Abiria wanusurika baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuteketea.

Abiria wanusurika baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuteketea.

321
0

Jumla ya abiria 41 wamenusurika kifo jioni ya leo baada ya basi walimokuwa wakisafiria kushika moto.

Mkasa huo wa mwendo wa saa kumi na moja jioni umelihusisha basi la kampuni ya Tahmeed lililokuwa likitoka Jijini Nairobi likileakea Mjini Mombasa.

Kamanda mkuu wa trafiki katika Ukanda wa Pwani Emmanuel Okanda amesema kwamba abiria wote wametolewa salama bila majeraha yoyote kabla ya moto huo mkali kuliteketeza kabisa basi lote.

Hakuna mali yoyote iliyookolewa kwenye mkasa huo kwani mizigo yote ya abiria imeteketezwa na kugeuzwa jivu.

Kiini cha moto huo hakijabainika huku Okanda akisema kwamba visa hivyo vya mabasi kuteketea katika hali tata hasa ya kutoka Mombasa vimekithiri.

Tukio hilo linajiri Siku mbili tu baada ya basi moja la kampuni ya Dreamline kuteketea katika hali tata katika eneo la Macknon road katika Kaunti ya Kwale kwenye barabara hiyo kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Jijini Nairobi.

Watu wawili wangali wanauguza majeraha mabaya ya moto katika hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani huku kiini cha mkasa huo kikisalia kitendawili.

Mkasa huo wa jioni ya leo umesababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Jijini Nairobi.