Home Swahili Hub Deni la trilioni 5.1 litaongeza gharama ya maisha –Haki Africa

Deni la trilioni 5.1 litaongeza gharama ya maisha –Haki Africa

315
0
[Mkurugenzi Mkuu wa Haki Africa Hussein Khalid akiwa afisini mwake. Picha/Hussein Mdune]

Mkopo wa Serikali kuu kutoka kwa mataifa ya nje ndicho kiini hasa cha kukwea kwa gharama ya maisha humu nchini.

Ni kufuatia deni hilo la zaidi ya kima cha shilingi trilioni 5.1 ndipo Serikali imeafikia kutekeleza ushuru wa asilimia 16 kwa mafuta yanayoingizwa humu nchini.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Africa Khalid Hussein amesema kwamba hali hiyo itazidi kumkandamiza Mkenya mashinani hasa ikizingatiwa kwamba kupanda kwa bei za mafuta kutasababisha kupanda kwa bei za bidhaa muhimu nchini.

Khalid amesema kwamba kama watetezi wa haki za kibinadamu nchini wametamaushwa mno na jinsi Serikali inavyoshindwa kuthamini maisha ya Kenya licha ya bunge la kitaifa kuongeza muda wa miaka miwili kabla ya nyongeza hiyo ya asilimia 16 ya ushuru kuanza kutekelezwa.

Khalid amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuipasisha sheria iliyopitishwa na bunge la kitaifa hivi majuzi ya kuzuia nyongeza hiyo ya ushuru kwa mafuta yanayoingizwa humu nchini.

“Tayari Mkenya mashinani anataabika mno kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, na nyongeza hii ya ushuru itaifanya hali hiyo kuwa mbaya hata zaidi,” akaongeza Khalid.

Tayari Waziri wa hazina ya kitaifa Henry Rotich aliongeza ushuru huo akisema kwamba ni sharti utekelezwe ili kuiwezesha Serikali kumudu gharama ya kuendeleza shughuli mbalimbali na kutoa huduma msingi kwa Wakenya.

“Hatujafurahishwa na hatua ya Rotich sambamba na Mamlaka ya ushuru nchini KRA, Wakenya wanahangaika na ni lazima swala hilo liangaziwe kwa kina kwa kumzingatia mwanachi mashinani,” akaongeza Khalid.

Vile vile, Bunge la kitaifa limedhihirisha wasiwasi wake kuhusu utata huo na kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuizuia nyongeza hiyo ya ushuru kwa mafuta yanayoingizwa nchini.

Nyongeza hiyo tayari imeathiri shughuli za uchukuzi nchini huku Wakenya wakilihisi joto la nauli kupanda mara dufu katika huduma ya uchukuzi wa umma.

Katika uhalisia wa mambo, lita moja ya mafuta ya petroli katika Kaunti ya Mombasa inauzwa kwa shilingi 124 kinyume na bei ya awali ya shilingi 105, dizeli ikiuzwa kwa shilingi 110 ikilinganishwa na bei ya awali ya shilingi 95, mafuta ya taa yakiuzwa kwa shilingi 93 ikilinganishwa na bei ya awali ya shilingi 70.