Home Swahili Hub Mabanda ya filamu kuchangia kuenea kwa TB.

Mabanda ya filamu kuchangia kuenea kwa TB.

249
0
[Afisa anayesimamia kitengo cha tiba ya TB katika maeneo ya Kisauni na Nayli Kunti ya Mombasa Bi Mary Katana. Picha/Maxwell]

Msongamano wa wanaume katika mabanda ya filamu msimu huu wa michuano ya kombe la dunia huenda ukachangia katika maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Hali hiyo inatokana na ukosefu wa hewa safi katika mabanda hayo sawa na msongamano wa watu wengi ili kutazama dimba hilo la mwezi mzima nchini Urusi.

Afisa anayesimamia kitengo cha hamasa na tiba ya maradhi ya kifua kikuu katika maeneo bunge ya Kisauni na Nyali Bi Mary Katana amewataja wanaume kama walio katika hatari ya maambukizi hayo hasa kutokana na tabia yao ya kukongamana pamoja katika mabanda hayo na maeneo mengine ya burudani.

Kulingana na Bi Katana, huenda baada ya michuano ya kombe la dunia visa vya maambukizi ya ugonjwa wa TB vikaongezeka katika eneo hilo kutokana na mfumo huu wa msimu.

“Sio msongamano tu katika mabanda hayo bali pia wanaume wanakisiwa kutojishughulisha na ulaji bora wa vyakula vilivyo na virutubisho ikilinganishwa na wanawake hivyo basi kujiweka katika hatari ya maambukizi,” akadokeza Bi Katana.

Mtaalam huyo wa tiba ya kifua kikuu hata hivyo ametaja moja wapo wa changizo la maambukizi ya TB haswa katika gereza la Shimo la Tewa ni uhaba wa nafasi na msongamano wa wafungwa kwa upande za wanaume, wanawake na watoto.

“Hata hivyo, kitengo cha kukabiliana na TB kinaendeleza hamasa mashinani, matibabu kwa wanaougua na kuwafutialia wale waliyo kwenye orodha ya wagonjwa wa TB ili kuhakikisha wanakamilisha matibabu,” akasisitiza Afisa huyo.

Bi Katana amewataka wakaazi wa Kisauni na Nyali kuwa makini mno na afya zao na kutembelea hospitali za umma ili kupimwa TB akidokeza kwamba kukohoa majuma matatu mtawalia na kutokwa na jasho jingi nyakati za usiku huenda ikawa ishara kamili ya ugonjwa wa TB.

Amesema maeneo ya Kisauni na Nyali yana zaidi ya wagonjwa elfu moja wa kifua kikuu huku 28 kati yao wakiugua TB sugu inayohitaji tiba maalum ya hadi mwaka mmoja na jumla ya sindano nane kupona.