Home Swahili Hub Mchakato wa kuibadili katiba ni njama ya Viongozi wa kisiasa

Mchakato wa kuibadili katiba ni njama ya Viongozi wa kisiasa

719
0
[Askofu wa Kanisa la Ushindi Baptist Joseph Maisha. Picha/Hussein Mdune]

Viongozi wa kidini katika Kaunti ya Mombasa wameutaja mchakato wa kuifanyia marekebisho katiba kama njama ya viongozi wa kisiasa ya kujinufaisha maslahi yao binafsi.

 

Kulingana na Askofu wa Kanisa la Ushindi Baptist katika eneo la Likoni Joseph Maisha, mchakato huo kamwe hauna nia yoyote ya kumsaidia Mkenya mashinani.

 

Kiongozi huyo wa kidini ameongeza kwamba mbinu hiyo ina lengo la kubuni nafasi za uongozi kwa wanasiasa na kamwe sio kuimarisha hali ya maisha ya Mkenya mashinani.

 

Askofu Maisha amesema kwamba taifa hili limebeba mzigo wa madeni na linalopaswa kushughulikiwa na viongozi hao kwa sasa ni kuibuka na mikakati ya kulilipa deni hilo.

 

“Kama Viongozi wa kidini tunachotaka kuona kwa sasa ni majadiliano kuhusu jinsi ya kuimarisha uchumi wa taifa, jinsi ya kuwaunganisha Wakenya na kukomesha siasa za ukabila na ulafi,” akaongeza Askofu huyo.

 

Maisha ameweka bayana kwamba mchakato huo umechukua mkondo wa siasa na unalenga kuligawanya taifa hili hata kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

 

“Ni kipi tunachotaka kubadilisha kwenye katiba ambayo hadi sasa hatujaonyesha ari yoyote ya kuichambua, kuitekeleza wala kuizingatia kikamilifu?” akauliza Kiongozi huyo wa dini.

 

Askofu Maisha amesisitiza umuhimu wa Viongozi wa kisiasa kulitazama kwa undani swala la maendeleo na jinsi ya kuimarisha hali ya maisha ya Wakenya mashinani na wala sio kuendeleza siasa zisizokuwa na malengo msingi kwa Mkenya.

 

Amewataka wananchi kuwa makini mno kuhusiana na mchakato huo wa kuigeuza katiba ya sasa na kujitenga na wanasiasa ambo lengo lao kuu na kuligawanya taifa hili, hali ambayo anasema itazalisha chuki za kisiasa, kikabila na kidini nchini.

 

Amewataka Viongozi wakuu Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kutathmini jinsi deni la kima cha shilingi trillion 5.1 litakavyolipwa ili kumpunguzia Mkenya gharama ya juu ya maisha.

 

Tangu kuzuka kwa mchakato huo wa kuirekebisha katiba, taifa limeshuhudia mabishano makali mno ya kisiasa na ambayo ni bayana yamewagawanya Wakenya.