Home Swahili Hub Mwanahabari wa Mombasa ashinda tuzo la makala bora barani Afrika.

Mwanahabari wa Mombasa ashinda tuzo la makala bora barani Afrika.

505
0

Mwanahabari nguli wa kutoka idhaa ya Radio Rahma Mjini Mombasa Ruth keah ametunukiwa tuzo ya makala bora barani Afrika.

Ruth Keah ambaye pia ni mhariri katika idhaa hiyo ya Rahma, aliibuka kidedea katika mashindano ya kwanza ya waandishi wa habari katika kitengo cha kukabiliana na hatari ya maafa wakati wa majanga yaliyoandaliwa mjini Tunis Nchini Tunisia.

Makala hayo yaliyokuwa yamesheheni utafiti wa kina, ubunifu katika uandishi na utayarishi wake sawia na uweledi ulioweka wazi hali halisi ya athari za mabadiliko ya anga kutokana na harakati za wanadamu zinazokisiwa kuchangia pakubwa kukauka kwa Mto Voi ulioko katika kaunti ya Taita Taveta.

Ushindi huo katika kitengo cha redio ulikuwa na upinzani mkali ikizingatiwa kuwa zaidi ya makala 100 yaliwasilishwa na wanahabari tofauti kutoka mataifa mbali mbali barani Afrika na hata nchi chini ya milki za Kiarabu.

Hata hivyo mwanahabari huyo alielezea mshtuko alioupata pale alipoteuliwa kuwa mshindi wa makala hayo akidai kuwa kamwe hakutarajia.

“Moyo wangu ulisimama kwa nukta sekunde niliposikia jina langu likitangazwa kama mshindi, sikudhania wala kutarajia kutokana na ushindani mkali katika kitengo hiki,” alisema Ruth akiwa na tabasamu usoni.

“Shukrani zote ni kwa Mungu pamoja na kikosi kizima cha Radio Rahma kwa kunipa nafasi na usaidizi kufanikisha makala haya na hii leo kushinda tuzo hili,” aliongeza Ruth.

Aidha Mwanahabari huyo alibaini changamoto alizopitia katika kutayarisha makala hayo licha ya kumpa fursa ya kutangamana na wananchi mbali mbali na kujifunza mengi katika tasnia ya uwanahabari.

Miongoni mwa tuzo alizopata katika ushindi huo ni kikombe pamoja na safari ya kwenda Geneva mwaka ujao kushiriki katika kongamano la kimataifa la washikadau linalotarajiwa kuangazia mbinu za kukabiliana na majanga na kubadilika kwa hali ya anga duniani.

Baadhi ya tuzo zilizofika nchi za afrika mashariki ni kwa wanahabari kutoka taifa la Uganda na Misri.

Itakumbukwa kuwa mwanahabari Ruth Keah alitunukiwa tuzo la mtangazaji bora kwenye kitengo cha ICT sawia na watatu bora katika kitengo cha biashara kwenye sherehe zilizoandaliwa na shirika la Wanahabari nchini Media Council Of Kenya tarehe 3 August Mwaka huu.