Home Swahili Hub Mzozo wa ardhi wachacha, Mwavumbo-Kinango

Mzozo wa ardhi wachacha, Mwavumbo-Kinango

502
0
[Mwanasiasa wa Chama cha Jubilee Pwani Ali Mwatsahu akilizungumzia tatizo sugu la ardhi katika Ukanda wa Pwani. Picha/ Hussein Mdune]

Wakaazi wa eneo la Mwavumbo eneo la Kinango Kaunti ya Kwale wanaitaka Serikali kuu kuingilia kati mzozo wa ardhi unaozidi kupamba moto katika eneo hilo.

Hii ni baada ya Mfanyibishara mmoja kudaiwa kuivamia ardhi ya eneo hilo akidai ni mali yake kutokana na hali ya ardhi hiyo kuwa pambizoni mwa barabara ya reli ya kisasa SGR.

Wakaazi hao wakiongozwa na Mwanasiasa wa Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Mombasa  Ali Mwatsahu wameitaka Wizara ya ardhi kuingilia kati na kuutanzua mgogoro huo.

Kulingana na Mwanasiasa huyo, kipande hicho cha ardhi kilicho na ukubwa wa hekari elfu 30 kimekuwa kiini cha mzozo kati ya Wazee wa eneo hilo la Mwavumbo na Mfanyibiashara huyo.

“Bwenyenye huyo alivamia ardhi hiyo akiweka vigingi na kudai umiliki wa ardhi  hiyo,” akaongeza Mwatsahu.

Kulingana na Mwatsahu, ardhi hiyo ilitengwa na wazee wa eneo hilo la Mwavumbo miaka ya nyuma ili itumike katika kutoa mafunzo kuhusu kilimo na maswala mengine ya kijamii.

“Kufuatia ukame uliyokuwa ukishuhudiwa katika eneo hilo, wazee walikutana na kutoa kipande hicho ili kuendeleza shughuli za kilimo hakiwezi kunyakuliwa  mbele ya macho yetu,” akahoji Mwatsahu.

Hata hivyo, Mwanasiasa huyo amewalaumu baadhi ya Viongozi wa eneo la Pwani kwa kuendeleza ukandamizaji huo na unyakuzi wa ardhi bila ya kujali dhuluma na ukandamizaji anaopitia Mpwani.

Amewasihi Wakaazi wanaoishi pambizoni au kwenye ardhi zilizo na rutuba na zilizo katika hatari na kunyakuliwa kuwa makini mno na kusimama kidete ili kuitetea raslimali yao.

Mwatsahu hata hivyo ameitaja Serikali kama iliyo na jukumu katika kudhibiti unyakuzi wa ardhi Pwani akiitaka iliwajibikie tatizo hilo.

Tayari Kamishna wa Tume ya ardhi nchini Samuel Tarorei amefichua kwamba jumla ya visa 60 vya unyakuzi wa ardhi na dhuluma Pwani vimeripotiwa katika tume hiyo.

“Kwa sasa tunapokea lalama kuhusiana na swala la unyakuzi wa ardhi nchini na baada ya kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano, visa vyote ambavyo vitakuwa vimeripotiwa mbele ya tume hii tutaviandamana vilivyo na kuvitanzua,” akawahakikishia Wakaazi wa Pwani.