Home Swahili Hub NEMA yatakiwa kudhibiti vumbi kali Portreitz

NEMA yatakiwa kudhibiti vumbi kali Portreitz

358
0

Mamlaka ya mazingira nchini NEMA imetakiwa kusitisha uchafuzi wa mazingira inayotokana na upanuzi wa bandari ya Mombasa katika eneo la Portreitz huko Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Wakaazi wa eneo hilo wamelalamikia vumbi kali wanalosema limewasababishia maradhi ya macho, vifua na mapafu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kaunti ya Mombasa Mohammed Jahazi, Wakaazi hao wamesema kwamba hali hiyo imezidi kuwa mbaya kila uchao, huku vile vile kuwepo kwa kampuni za uchukuzi katika eneo hilo kukichangia athari za kiafya hata zaidi.

Jahazi amesema kwamba uhifadhi wa makasha katika kampuni hizo za uchukuzi umechangia kelele za usiku kucha, huku upanuzi wa bandari ya Mombasa ukichangia vumbi kali.

Jahazi amesema kwamba baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wamelazimika kuhama makwao na kusaka hifadhi kwengine kufuatia hali hiyo tata ya kimazingira.

“Hali hii imefikia viwango vya kutisha, tunakula vumbi na kulala kwenye vumbi, ni sharti hatua zichukuliwe ili kudhibiti uchafuzi huu wa mazingira,” akaongeza Bwana Jahazi.

Kulingana na mkongwe huyo katika ulingo wa siasa, ni sharti Serikali kuu itekeleze miradi yake kwa kumzingatia Mwananchi mashinani, akisema kwamba licha ya wao kulalamika, serikali imewapuuza.

 

“Hatupingi miradi ya Serikali kwa sababu tunafahamu bayana ni maendeleo ya taifa lakini miradi hii imetuathiri pakubwa kiafya,” akahoji Jahazi.

Amesema kwamba hali ni tata hata zaidi katika hopistali ya Portreitz katika eneo hilo la Changamwe ambapo vile vile imeathirika na vumbi hilo.

Jaazi ameitaka mamlaka ya mazingira nchini NEMA kushirikiana na Serikali ya Kaunti ya Mombasa sambamba na ile kuu ili kuhakikisha kwamba maslahi ya wakaazi wa eneo hilo la Portreitz yanapewa uzito unaostahili.