Home Swahili Hub Rwanda yapiga marufuku kutangaza biashara za kiganga

Rwanda yapiga marufuku kutangaza biashara za kiganga

602
0

Serikali ya Rwanda kupitia wizara ya afya nchini humo imepiga marufuku kutangaza biashara ya madawa ya kiasili kwa kutumia picha, mabango au pia kutumia vipaaza sauti barabarani kote nchini Rwanda.

Kulingana na taarifa kutoka kwa wizara ya afya nchini humo, imeashiria kuwa biashara ya madawa ya kijadi au kiasili imeonekana kushamiri kutokana na waganga wengi wa jadi kutumia vibaya vyombo vya habari kuwasilisha jumbe na matangazo yao yanayodaiwa kupotosha wananchi.

Vyombo vya habari ikiwemo magazeti, mitandao ya kijamii , redio na televisheni vimekabiliwa na ilani hiyo ya kutopitisha vipindi au kupeperusha matangazo yoyote ya biashara kuhusu uganga wa kijadi.

Marufuku hiyo imepokelewa na hisia mseto nchini humo huku baadhi ya waganga wa kijadi wakidai kuwa hatua hiyo itawakandamiza wale waliokuwa wakiendesha biashara kwa uhalali au uhalisia wa tiba za kiasili.

Kwa mda sasa, waganga nchini humo wamekuwa wakipishana huku kila mmoja akitangaza umaarufu wake kutibu magonjwa sugu wanayosema kwamba yamekosa tiba ya kizungu.

Wengine walionekana kuvuka mipaka kwa kutangaza kuwa wanatoa madawa ya Baraka na hata kutibu umaskini huku wengine wao wakijitoa kimasomaso wakitangaza wazi kuwa wachawi.

Hata hivyo, Mashirika ya waganga wa jadi pia yameunga mkono uamuzi wa wizara ya afya yakisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa katika kuweka utaratibu mzuri na imara wa utendaji kazi wa waganga wa jadi na kuwagundua wanaopotosha umma.