Home Swahili Hub Sekta ya utalii yatarajiwa “kufufuka”-waziri Balala

Sekta ya utalii yatarajiwa “kufufuka”-waziri Balala

509
0
[waziri balala pamoja na viongozi wengine wakiwalaki watalii katika uwanja wa ndege-picha/kwa hisani]

Huenda sekta ya utalii ikaimarika pakubwa nchini hususan katika eneo la pwani kutokana na ongezeko la safari za ndege za kigeni.

Haya ni kulingana na waziri wa utalii Najib Balala akielezea mafanikio yanayotarajiwa kutokana na mkataba wa maelewano walioafikiana na mataifa ya kigeni katika kusahilisha safari za ndege.

Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Moi wakati wa mapokezi ya watalii zaidi ya 120 kutoka nchi ya Uholanzi, Balala amebaini kuwa mpango huo wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hadi jijini Mombasa umefungua ukurasa mpya utakaoboresha sekta hiyo ya utalii.

Watalii hao waliowasili kwa hisani ya kampuni ya ndege ya TUI  yenye makao yake nchini Uholanzi, ni miongoni mwa mazao yaliyotokana na mazungumzo ya kuafikia mkataba wa maelewano yaliyoanzishwa mnamo mwaka wa 2016.

Balala amebaini kuwa maafikiano hayo yamesaidia pakubwa katika kuimarisha idadi ya watalii wanaozuru sehemu mbali mbali za kujivinjari ukanda wa pwani huku akitaja kuwa takriban watalii elfu 55 kutoka mataifa ya kigeni wameripotiwa kuzuru humu nchini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Aidha waziri huyo amedokeza kuwa ndege 15 za watalii kutoka mataifa ya kigeni zinatarajiwa kuwasili humu nchini kila wiki msimu huu ikilinganishwa na idadi ya ndege 9 walizopokea mwaka jana.

Hata hivyo waziri Balala aliongezea kuwa mazungumzo hayo yameelekezwa katika mataifa mengine ya bara yuropa ili kuona mahusiano ya kibiashara haswa katika sekta ya usafiri na utalii yanapanuka.

“kupitia wizara yangu,makubaliano na nchi ya Uingereza yamefikia mkondo wa mwisho. Tunatarajia ndege za watalii kutoka nchi hiyo kuanzia mwezi novemba mwaka ujao,” alisema Balala.

“vile vile tumeeza kukubaliana na Uholanzi ,Urusi ,Italy na Poland hatua ambayo inapania kuongeza idadi ya watalii wanaozuru ukanda wa pwani na nchi nzima kwa jumla,” aliongezea waziri.

Licha ya makubaliano hayo ya ndege za moja kwa moja hadi humu nchini kuonekana kuleta afueni kwa watalii kwa jumla, baadhi walionekana kukerwa na jinsi ya baadhi ya huduma zinavyotekelezwa wanapowasili katika viwanja vya ndege humu nchini.

Lalama zilielekezwa kwa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kwa kutokuwa na mfumo thabiti wa kuepusha milolongo kwa watalii hivyo basi kutakiwa kuboresha huduma zao.

Wengi wamelalamikia kupoteza mda mrefu katika viwanja vya ndege wakati wa ukaguzi wa mizigo sawia na uthibitisho wa vyeti vya usafiri ndiposa kuitaka serikali kupitia wizara ya utalii kuliangazia swala hilo.

kwa upande wake Mwenyekiti  wa shirikisho la sekta ya utalii nchini Mohamed Hersi amepongeza hatua na jitihada zinazowekwa na wizara ya utalii nchini katika kuimarisha sekta hiyo, huku akihimiza serikali kuwekeza zaidi ili kuona kwamba pato linalotokana na sekta hiyo inasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.

Hata hivyo ameitaka serikali kupunguza viwango vya ushuru wanavyotozwa watalii akitaja kama njia moja wapo ya kuvutia wageni zaidi humu nchini.