Home Swahili Hub Serikali yatakiwa kumtimua mkuu wa IPSOS nchini

Serikali yatakiwa kumtimua mkuu wa IPSOS nchini

284
0
[Mwanasiasa wa Jubilee Mjini Mombasa akiwahutubia Wanahabari. Picha/Hussein Mdune]

Mwanasiasa wa Chama cha Jubilee Abdi Daib ameitaka Serikali kuinyang’anya kibali kampuni moja ya utafiti sawa na kumtimua Mkurugenzi wake mkuu humu nchini.

Daib aidha amemtaka Waziri wa maswala ya ndani nchini Dakta Fred Matiang’i kumtimua Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya utafiti ya Ipsos Synovate Tom Wolf baada ya kampuni hiyo kutoa matokeo yake ya utafiti kuhusu ufuisadi humu nchini.

Katika ripoti hiyo, Naibu Rais William Ruto aliorodheshwa nambari moja kwa ufisadi akiwa na asilimia 33 huku nyuma yake akifuatia Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Bi Anne Waiguru aliyepata asilimia 31.

Kulingana na Mwanasiasa huyo wa Kaunti ya Mombasa utafiti huo ulikuwa umechochewa kisiasa na kwa kiwango kikubwa unalenga kuligawanya taifa hili kisiasa.

Daib ameongeza kwamba utafiti huo una malengo makuu ya kuzima ndoto ya kisiasa ya Naibu rais anayepania kupigania urais pindi ifikapo mwaka wa 2022.

“Kwa kweli utafiti huu hauna msingi wowote, ni njama ya kisiasa dhidi ya Naibu rais William Ruto na kamwe hatutakubali,” akahoji Daib.

Daib ameitaka idara inayohusika na usimamizi wa makampuni ya utafiti nchini kufutilia mbali laseni ya kampuni ya Ipsos Synovate na kumtimua Wolf nchini ambaye ni Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo.

Katika utafiti huo, vile vile Rais Uhuru Kenyatta alipata alama 11 za ufisadi, japo asilimia 51 ya wale waliyohojiwa walidhihirisha imani yao kwamba Rais Uhuru Kenyatta ana nia njema katika vita dhidi ya ufisadi.

Utafiti huo umemhusisha moja kwa moja Bi Anne Waiguru na kashfa ya kima cha shilingi milioni 791 fedha za hazina ya Shirika la huduma ya vijana kwa taifa nchini NYS wakati alipokuwa Waziri wa Ugatuzi.

Utafiti huo vile vile ulimhusisha Naibu rais William Ruto na kashfa ya kuingizwa kwa mahindi humu nchini.

Baadhi ya kashfa ambazo Wakenya wanazitambua barabara ni ile ya NYS, ya mahindi, sakata ya sukari iliyo na zebaki, ile ya bodi ya nafaka nchini yaani National Cereals and Produce Board-NCPB, sakata ya ufisadi iliyoikumba Kampuni ya usambazaji nguvu za umeme nchini Kenya power miogoni mwa kashfa nyingine nyingi za rushwa humu nchini.