Home Swahili Hub Utata wagubika kifo cha Afisa wa Polisi, Mombasa

Utata wagubika kifo cha Afisa wa Polisi, Mombasa

271
0
[Benjamin Wafula Msimamizi katika hospitali ya Jocham. Picha/Maxwell Ngala]

Mabishano makali yamezuka kufuatia kifo cha Afisa wa polisi wa eneo la Kisauni Kaunti ya Mombasa Njoroge Thuo aliyedungwa kisu tumboni na genge la majambazi katika mtaa wa Magodoroni ambapo mashirika ya haki za kibinadamu sasa yanataka uchunguzi wa kina na wa dharura uidhinishwe.

Mashirika hayo yakiongozwa na Haki Afrika yanashikilia kwamba maafa ya Thuo yangezuiliwa iwapo hospitali ya kibinafsi ya Joacham alikokimbizwa Afisa huyo ingewajibika katika kuyaokoa maisha yake.

Katika taarifa aliyoituma katika vyombo vya habari siku ya Jumatatu, Mkurugenzi mkuu wa  Shirika hilo Hussein Khalid amesema kwamba ni lazima tukio hilo lichunguzwe na matokeo yake kuwekwa wazi kwa kuwa limezungukwa na utata mwingi mno.

Mtetezi huyo wa haki za kibinadamu vile vile ametaka huduma zote za kiafya zinazotolewa hospitalini humo zikaguliwe ili kubaini iwapo ni bora ni zinastahili kwa wakaazi wanaozuru ili kutafuta tiba.

Khalid amefichua kwamba maelezo waliyokusanya kutoka kwa Afisa mkuu wa polisi wa Kisauni Sangura Msee na yale yaliyotoka kwa Msimamizi wa hospitali  hiyo ya Joacham Benjamin Wafula yanakinzana, ishara kamili kwamba kifo cha Thuo kilichangiwa na utepetevu.

“Hapa tunazungumzia kifo cha Afisa wa Polisi wala hatumlaumu yeyote, ni lazima tubaini ukweli kuhusu tukio hilo,” akasema mtetezi huyo wa haki za kibinadamu.

Khalid amezitaka idara husika ikiwemo ile ya usalama na Maafisa wa Wizara ya afya kuharakisha uchunguzi huo ili ukweli kuhusu kifo cha Thuo ubainike.

“Sisi hatutapoumzika hadi pale tutakapofahamishwa majibu ya uchunguzi kuhusu kifo cha Thuo, na iwapo kilisababishwa na utepetevu basi sheria ichukue mkondo wake,” akasisitiza Khalid.

Kauli ya Khalid inajiri baada ya Afisa mkuu wa polisi wa eneo la Kisauni Sangura Msee kudai kwamba kifo cha Thuo kilitokana na utepetevu na kejeli za Wahudumu wa afya katika hospitali hiyo ya kibinafsi ya Joacham.

Hata hivyo,  Msimamizi mkuu wa hospitali hiyo Benjamin Wafula amepinga madai ya Msee akisema kwamba Madaktari wa hospitali hiyo walijizatiti kumpatia marehemu Thuo tiba ya dharura kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya Premier Mjini Mombasa alipofariki kabla ya kuwasili hospitalini humo.

Wafula amekanusha kwamba Madaktari walimlazimisha Thuo aliyekuwa akivuja damu nyingi kutoa kitambulisho chake cha kitaifa na kadi ya hazina ya matibabu ya umma NHIF kabla ya kuhudumiwa, akaitaja kauli ya Msee kama ya uongo.