Home Swahili Hub Wako wapi? Wauliza watetezi wa haki, Pwani

Wako wapi? Wauliza watetezi wa haki, Pwani

376
0
[Waandamanaji wakidhihirisha huzuni wakati wa kuwakumbuka watu waliyopotezwa katika hali tata siku ya Alhamis Mjini Mombasa. Picha/ Hussein Mdune]

Zaidi ya watu 100 wamepotea katika hali tata mno Kaunti ya Mombasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katika siku ya kumbukumbu kwa watu waliyopotezwa katika njia tata inayoadhimishwa kila siku ya 30 ya Mwezi Agosti kila mwaka kote ulimwenguni, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la Haki Afrika Hussein Khalid amesema kwamba asilimia 90 ya wahanga hao wako chini ya umri wa miaka 35.

Akiongoza maandamano ya amani katika Kaunti ya Mombasa siku ya Alhamis katika kumbukumbu hizo, Khalid amesema kwamba licha ya watetezi hao kuilalamikia Serikali kuhusiana na ukiukaji huo mkubwa wa haki za kibinadamu, hakuna hatua zozote mwafaka zilizochokuliwa ili kuidhibiti hali hiyo.

Khalid amefichua kwamba familia nyingi katika Kaunti hiyo ya Mombasa zinapitia mateso ya kisaikolojia kutokana na kupotezwa kwa walezi wa familia hizo.

“Tunaitaka Serikali iingilie kati ili kuyakomesha madhila haya na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu, ni nani anayewapoteza watu hawa?” akauliza Khalid.

Akitoa kauli yake katika msafara huo wa siku ya ALhamis Mjini Mombasa Mbarak  Khalid ambaye ni  mzazi wa kijana Husni Mbarak mwenye umri wa miaka 18 aliyepotea mapema mwezi Mei Mwaka huu ameikashfu zaidi Serikali kwa kushindwa kuwalinda Wananchi.

Mbarak amedhihirisha masikitiko yake kuhusiana na jinsi mwanawe alivyonyakuliwa katika eneo la Majengo Kaunti hiyo ya Mombasa akiongeza kwamba hadi sasa kamwe hajamuona mwanawe.

Hata hivyo, akiyapokea matakwa ya Mashirika hayo, Mshirikishi mkuu wa Ukanda wa Pwani Bernard Leparmarai ameyataka Mashirika hayo kukoma kuwasingizia Maafisa wa polisi kwamba ndio wahusika wakuu katika visa hivyo.

Leparmarai amewataka Watetezi hao wa haki za kibinadamu kushirikiana na Idara ya usalama Pwani katika kulinda hali ya usalama na kukomesha dhuluma hizo, huku akiwaahidi Watetezi hao kwamba Maafisa wa usalama wanachunguza kwa kina matukio hayo.

“Ni kweli familia nyingi zinapitia wakati mgumu lakini zinapaswa kuwa na uvumulivu na kushirikiana nasi kadri tunavyoendeleza uchunguzi kuhusiana na matukio hayo,” akaweka wazi Leparmarai.